Wednesday, November 9, 2011

Mjadala wa Katiba Mpya: mambo bado moto

November 10, 2011



Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Pd Anthony Kakunde, akitoa neno kabla ya mjadala wa katiba mpya

Na Elias Mhegera

IMEJIDHIHIRISHA bado kuna changamoto kadhaa katika mjadala wa katiba kutokana na mjadala wa viongozi wa madhehebu ya dini mbali mbali katika kongamano lilomalizika wiki jana (Jumatano)

Mjadala huo uliandaliwa na Baraza la Madhehebu ya Dini kwa Ajili ya Amani Tanzania (IRCPT), kwa ushirikiano na Mfuko wa Amani na Demokrasia wa Konrad Adenauer (KAS), kutoka nchini Ujerumani.

Mjadala huo wa katiba uliofanyika mwanzoni mwa wiki jana katika Ukumbi wa wa Kimataifa wa Mikutano Dar es Salaam (DICC), ulimshuhudia mgeni rasmi katika tukio hilo balozi wa Ujerumani nchini Bw Klaus-Peter Brandes akimimina sifa kwa Tanzania kutokana na kudumisha amani. Alisema amani iliyopo nchini inatokana na wosia uliochwa na mwalimu Julius Nyerere ambaye ni mwanzilishi wa taifa hili.

Alisema kama ilivyokuwa kwa Konrad Adenauer aliyepata kuwa kiongozi mahiri nchini Ujerumani mwishoni mwa miaka ya 40, busara, uadilifu na moyo wa kuwatumikia wananchi ndiyo msingi wa kuheshimika kwa viongozi katika taifa lolote duniani.

Awali katika hotuba yake ya kuwakaribisha wajumbe wa kongamano hilo Mkurugenzi wa KAS-Tanzania Bw. Stefan Reith alisema Tanzania imetunukiwa amani ya kuigwa kutokana na viongozi wa madhehebu mbali mbali ya dini kuweza kukaa kwa pamoja bila kubaguana ili kufikia muafaka juu ya masuala muhimu yanayoihusu nchi yao.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini IRCPT, Jaji Mstaafu Raymond Mwaikasu aliwasihi viongozi wa dini waendelee kuwa na ujasiri wa kuijadili katiba kwa uwazi zaidi kwa sababu hiyo ndiyo inatoa mwongozo muhimu wa jinsi ya kuongoza nchi.

Aliwaondoa hofu hiyo kutokana na kuwepo kauli kutoka kwa viongozi wa kisiasa zinazowaonya kwamba wasichangaye dini na siasa, “ kukemea maovu au kujadili katiba siyo kuchanganya dini na siasa, changieni hoja bila woga huku mkifahamu kwamba mnao wafuasi wengi nyuma yenu kwa hiyo mchango wenu ni muhimu sana,” alisisitiza jaji huyo.

Kongamano hilo lilipata uwakilishi mzuri kutoka katika taasisi zote za madhehebu ya dini zikiwamo Ofisi ya Mufti Mkuu Zanzibar, Bakwata na Taasisi ya Wanataaluma Waislamu (TAMPRO). Kwa Upande wa Wakristu walikuwa Wakatoliki (TEC), Walutheri na Waanglikana (CCT), na Wapentekosti (PCT). Vile vile walikuwapo wawakilishi wa Bahaai na Budha.

Katika hatua nyingine wawezeshaji katika konagamano hilo Wakili Francis Kiwanga ambaye alikuwa mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki na Binadamu (LHRC) hadi hivi karibuni na Bw Deus Kibamba ambaye ni mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba.

Akiirejea historia ya katiba Tanzania Bw Kibamba alisema kwamba ingawaje wakoloni wa Kiingereza ndiyo waliacha katiba ya kwanza hapa nchini lakini katiba hiyo ilifanyiwa marekebisho mara kadhaa ili kukiji matakwa ya watawala na hatimaye ‘kuharibiwa’ rasmi kwa mara ya kwanza pale nchi ilipogeuzwa kuwa ya mfumo wa chama kimoja hapo mwaka 1965.

Baada ya hapo ilifikia hata mgombea binafsi naye akakataliwa hali iliyodidimiza uhuru wa watu kuchagua kile wanachokiamini. Alisema ukomo wa uharibifu huo ni pale mwaka 1977 ambapo jopo liloteuliwa kuunda katiba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), liligeuka kuwa jopo la kuunda katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Naye Bw Kiwanga aliziunga mkono hoza hizo kwa kiwango kikubwa lakini aliongeza kwamba mchakato ambao Watanzania wanaupigania siyo wa kurekebisha katiba iliyopo isipokuwa wa kuundwa kwa katiba mpya. Alidai kwamba katiba zote zilizotangulia zilipoteza uhalali wa kisiasa kwa sababu hazikuwashirikisha wananchi katika uundwaji wake.

Lakini akichangia hoja hiyo Jaji Mstaafu Mwaikasu alisema uwezekano wa kuundwa kwa katiba mpya upo lakini kwa kuunda Bunge la Katiba au Mkutano wa Taifa wa Kuunda Katiba Mpya. Hoja hiyo iliungwa mkono na Profesa Mstaafu wa Sheria Josephat Kanywanyi aliyesema Ibara ya 98 ya katiba iliyopo sasa ilikuwa inazuia uwezekano wa kuundwa kwa katiba mpya kabla ya kutunga sheria mpya ya uundaji huo.

Nao wajumbe kutoka Zanzibar walisema kwamba katiba mpya ni lazima iitambue Zanzibar kama nchi badala ya kuiona kama ni mkoa kama ilivyo kwa sasa. Hoja hiyo ilionekana kuvuta hisia za watu kutoka kila upande hususani wa Tanzania Bara ambao walishangaa kwamba malalamiko yamekuwa yakitokea mara nyingi upande wa Visiwani.

Bila kujali itikadi za kidini wala upande wa Muungano wanakotoka wajumbe takribani wote waliochangia mada walidai kwamba rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana madaraka makubwa sana ambayo yanahitaji kupunguzwa ili kuondoa uwezekano wa udikteta na matumizi mabaya ya madaraka.

Mjumbe Dkt. Paul Shemsanga kutoka Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (PCT), alidai kwamba Bunge la Tanzania limeshindwa kutunga sheria na badala yake limebakiza kuidhinisha Miswaada inayotoka Serikalini ili kuwa sheria kamili. Hoja hiyo iliungwa mkono na Sheikh Ali Saidi Mosse mwakilishi wa Jumuiya ya Waislamu ya Ahmadiyya ambaye pia alisema katiba mpya ianze kwa kumtambua Mungu.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania Pd Anthony Makunde waliwaasa viongozi wa madhehebu ya dini kuwahamasisha waamini katika dini zao kuchangia kwa kina mara mjadala wa kukusanya maoni kwa ajili ya katiba utakapoanza rasmi kwa sababu katiba ni mali ya Watanzania wote.

Naye Mratibu wa KAS, Bw Richard Shaba ameahidi kwamba taasisi yake itachapisha kitabu kutokana na mjadala huu. Pia amewaomba Watanzania kutoka katika kila kada kusoma vitabu vinavyohusu masuala ya demokrasia na utawala bora ili kufahamu kwa kina jinsi ambavyo nchi yao inaongozwa.

Huku akiungwa mkono na msaidizi wake Bw Erasto Ndeuka aliyesema tayari taasisi yake imekwisha chapisha vitabu mbali mbali vinavyohusu elimu ya uraia na mijadala ya katiba inayoendelea. Wawili hao walizungumzia kitabu chenye kurasa 58 kilichotokana na mjadala wa wanaharakati, wasomi na wadau wengine uliofanyika DICC April 12, mwaka huu.

Jina la kitabu hicho “Muswada wa Mapitio ya Katiba ya Nchi wa Mwaka 2011”, ni kiashiria kwamba mawazo ya wadau wote ikiwa ni pamoja na asasi za kiraia, wanaharakati wa kupigania haki za binadamu na vyombo vya habari viliyaweka pamoja mawazo yao ili kutoa chachu kwa wadau wengi ambao hawakupata mwanya wa kushiriki midahalo ya awali.

Mjadala huo uliozaa kitabu hiki uliandaliwa na taasisi inayo ratibu mpango ya maendeleo Tanzania yaani Tanzania Development Initiative Programme (TADIP), kwa ushirikiano na taasisi ya KAS.

Wazungumzaji wakuu katika mjadala huo wa mwezi Aprili walikuwa Profesa Chris Maina, mhadhiri wa sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Bw Bashiru Ally wa idara ya siasa kutoka chuo hicho. Wengine ni Bw Steven Mmbogo, meneja wa programu TADIP. Mwenyekiti wa mdahalo huo alikuwa Bi Rose Mwakitwange, mkurugenzi mtendaji mstaafu wa Habari Corporation.

No comments: