Wednesday, September 28, 2011

Madini na Nishati vipi?

FEMINIST ACTIVIST COALITION
(FemAct)

C/O Mtandao wa Jinsia Tanzania ( TGNP) S.L.P 8921 Dar es Saalam,Tanzania, Kituo cha Jinsia, Barabara ya Mabibo Mkabala na Chuo cha Usafirishaji (NIT) Simu +255 22 2443205; 2443450; 2443286 Selula: 255 754 784 050, Fax. 2443244, Barua Pepe info@tgnp.org, Tovuti www.tgnp.org
Julai 19, 2011

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Wizara ya Madini na Nishati Inaaibisha Taifa na Watanzania
Sisi Muungano wa Asasi za Kiraia zinazotetea Usawa wa jinsia, haki za binadamu, maendeleo na ukombozi wa wanawake kimapinduzi (FemAct) tumepokea kwa mshtuko, mshangao na masikitika makubwa, tuhuma kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Madini na Nishati, ameandaa mpango mahususi wa kukusanya pesa kutoka idara na wakala walio chini ya wizara yake, kwa ajili ya kuhonga Wabunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili wapitishe bajeti ya wizara hiyo.
Kwetu sisi wanaharakati, kitendo hiki ni ishara ya mambo makubwa zaidi yanayofanywa na baadhi ya viongozi wetu yanayosababisha kuendeleza ufukara na umaskini wa taifa letu na watu wake.
Kama tuhuma hizi ni za kweli, ni wazi kuwa mikakati mingine kama huu haikuanza mwaka huu, na hauwezi kuwa makakati wa Wizara ya Madini na Nishati pekee. Na kama hivyo ndivyo, basi Serikali ya Tanzania yote inanuka rushwa, na haina uhalali wa kuendelea kuongoza nchi, Serikali na Watanzania.
Uchambuzi yakinifu wa bajeti tunaofanya mara kwa mara sisi wanaharakati unatuonyesha jinsi gani rasilimali za taifa hili zinavyoendelea kufaidi wachache na kudumisha ufukara kwa wengi. Wanaharakati wa FemAct tunasema kwamba tatizo kubwa lisiishie kwenye kuwaadhibu waliyohusika na rushwa ya kupitisha bajeti. Tatizo ni pana zaidi na linahitaji tafakari pama ya kimfumo.
Sasa tumeamini kuwa Serikali inayoghubikwa na kuendeshwa kwa mfumo wa kuhongana miongoni mwa viongozi na watendaji wenye mamlaka ya kufanya maamuzi katika mihimili mikuu ya dola, ni Serikali ya hatari na isiyostahili kuenedelea kuwa madarakani. Serikali ya namna hii haiwezi kuwa na utashi wa kutumikia matakwa ya wananchi, isipokuwa kununuliwa na mafisadi.
Tatizo la Umeme
Tatizo la umeme sio la leo, ni suala ambalo limekuwa likipigiwa kelele kwa muda mrefu, Serikali imekosa mbinu na mikakati sahihi hadi kufikia hatua ya kutaka kubinafsisha Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco). Mikataba mingi michafu imeingiwa na Serikali kwa kutumia makampuni makubwa ya nje kama IPTL, Agreco, Songas, Richmond, Dowans na Net Group Solution. Hakika mbinu chafu zisingezaa matunda mema; tatizo la kukosa umeme limeongezeka mara dufu na wakati wote huu mwananchi masikini anaendelea kuteseka licha ya kulipia gharama zote anazobebeshwa na viongozi waongo na wahongwa.
Lakini katika mazingira haya ya rushwa, utapeli na ufisadi, Serikali imekosa utashi wa kushughulikia tatizo la umeme kwa kuzingatia mipango ya muda mrefu kama Miradi ya Makaa ya Mawe, Mchuchuma , Ngaka na Kiwira, ambavyo kwa pamoja ina uwezo wa kuzalisha megawati 1500 za nishati ya umeme ambayo inatosha kumaliza tatizo lililopo kwa takribani miaka mingi ijayo.
Inashangaza kuona taifa lenye rasilimali nyingi na miaka 50 baada ya uhuru likizalisha megawati 1034, wakati vyanzo vitatu vilivyotajwa hapo juu vingezalisha megawati 1500.
Mbali na mradi wa Mchuchuma, maporomoko ya mto Rufiji ya Stgiler’s Gorge, yana uwezo wa kuzalisha megawati zaidi ya 2,000 za umeme wa gharama nafuu. Lakini kila mwaka tunasikia kuwa mradi huu utaanza bila mafanikio matokeo yake tumeendelea kung’ang’ania kukodisha majenereta kutoka Ulaya na Marekani ambayo baada ya muda mfupi hushindwa kufanya kazi wakati mwingine kutuingiza kwenye mikataba michafu ya kifisadi.
Umeme kwajili ya nani?
FemAct tunataka kuona umeme ukiwa ni nishati muhimu kwa kila raia wa taifa hili, masikini wa kijijini na wa mjini, unaopatikana na kwa bei ambayo inaruhusu kila mwananchi anaweza kumudu gharama zake.
Ingawaje Tanzania ina utajiri mkubwa wa vyanzo vya nishati kama vile gesimoto(geothermal) nishati ya jua na upepo, pamoja na mkaa wa mawe, takribani asili mia 39% ya wakazi wa mijini na asili mia 2% ya wakazi wa vijijini wenye kufikiwa na umeme. Asilimia 10 ya kaya zote ndizo zinapata umeme kwa kupitia gridi ya taifa, na 1% tu ya kaya zote za Tanzania zinauwezo wa kutumia umeme kwa ajili ya kupikia. Wakati tukidai kwamba taifa limekumbwa na dharura kuwa gizani takribani nusu mwaka sasa, asili mia kubwa ya watanzania wako kwenye hali hii ya hatari takribani mika hamsini tangia tupate uhuru.
Iweje, miaka hamsini tangu tupate uhuru Taifa liko gizani? Iweje wazalishaji wakuu wa chakula, mazao ya biashara na walezi wa watoto wa taifa hili wawe kwenye giza kuu tangu bendera ya mkoloni kushushwa na kupandishwa kwa bendera ya Taifa huru? Iweje asili mia sabini hadi tisini ya Watanzania wamekuwa wakitegema aidha mkaa au kuni kwa ajili ya kupata nishati ya matumizi ya kaya?
Kwanini serikali itoe rushwa?
FemAct inaamini kuwa kuna sababu nyingine inayolazimisha Serikali kujaribu kutoa rushwa ili kupitisha bajeti ya Wizara ya Madini na Nishati; uwekezaji kwenye sekta ya madini na gesi asilia unatatizo kubwa.
Mfumo mzima wa mikataba, uwekezaji, usimamizi na uendeshaji wa shughuli za madini na gesi asilia hapa nchi unanuka rushwa, hakuna uwajibikaji na uwazi wake una mashaka. Watanzania hawanufaiki na madini na gesi asilia kutoka nchini mwao. Kuna migogoro mingi katika maeneo yanakochimbwa madini na gesi asilia baada ya wananchi kugundua ulaghai unaofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wawekezaji katika migodi ya madini na visima vya gesi asilia.
Kutokana na masuala yaliyoorodheshwa hapo juu, FemAct inataka Serikali ifanye marekebisho haraka kukidhi haja ya madai yafuatayo:-
1. Katibu Mkuu,Waziri ,Naibu wake kwa pamoja na watendaji wengine waliohusika kuchangisha fedha za kuwahonga wabunge waondolewe kazini na kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria haraka. Matendo yao ni kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.
2. Tunamtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awafute kazi watendaji hao mara moja na kuwachukulia hatua za kisheria ili iwe mfano kwa wahalifu wengine waliojificha katika ajira za Serikali.
3. Katika marekebisho ya bajeti ya Wizara ya Madini na Nishati Serikali ilete mikakati sahihi ya kulimaliza tatizo la umeme nchini. Serikali itaje vyanzo mbadala vya kuaminika vya kuzalisha umeme na sio kukodisha majenereta na kujiingiza kwenye mikataba ya kifisadi.
4. Serikali ieleze hatua dhabiti inazozichukua kuhakikisha vyanzo vya umeme wa upepo, nguvu ya jua,makaa ya mawe,maporomoko ya mto Rufiji, yanatumika ipasavyo kuzalisha umeme badala ya kuingia mikataba na makampuni ya kitapeli na kutegemea umeme wa mvua.
5. Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ieleze sababu za kushindwa kugundua mapungufu katika bajeti hiyo mapema na kuirudisha serikalini badala ya kupoteza muda wa umma.
6. Serikali ielekeze nguvu ya kufikisha umeme kwa wananchi wa vijijini na kwa bei rahisi ili kuongeza tija katika uzalishaji hasa kupitia kilimo na kuongeza ari ya kuanizishwa kwa viwanda vya kusindika mazao vijijini.
7. Serikali iwe wazi katika shughuli zake zote, hususan, mikataba ya madini, kufua umeme na kuzidua gesi asilia.
8. Serikali iunde tume huru kuchunguza mauaji ya hivi karibuni huko Nyamongo Mara na hii itamkwe ndani ya bajeti kwamba serikali itawalinda wananchi wake waishio jirani na migodi kwa mali zao na usalama wao. Vile vile serikali itoe tamko hatima ya mgodi wa Buhemba.
9. Serikali iweke wazi mikataba yote ya madini iliyopo ili kutoa fursa kwa umma kudadisi ikiwa ina maslahi kwa taifa. Zoezi la kuweka mikataba yote ya madini hadharani ni muhimu sana kuliko kuendelea kuvutia wawekezaji wapya katika sekta za nishati na madini ambazo zimeghubikwa na kashfa za ufisadi na uzembe.
Imetolewa Dar es salaam na:
Usu Mallya
Kny Sekretarieti ya Femact

No comments: