Na Elias Mhegera
HALI haikuwa ya kawaida pale washiriki wa mdahalo wa muswaada wa uanzishwaji wa katiba mpya walipotofautiana juu ya nini hasa kifanyike baada ya serikali kuonekana inadhamiria kuendeleza viraka katika katiba iliyopo kwa sasa.
Kelele za kusema ‘tunapotezewa muda’zilianza pale wanazuoni wawili Prof Chris Maina na mwenzake Bw Bashiru Ally wote wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walipoanza kuupitia muswaada huo kipengele kwa kipengele na kujiridhisha kwamba serikali hain a lengo la kuunda katiba mpya bali kuitrejea iliyopo ambayo tayari imepigiwa sana kelele na makundi mbali mbali ya kijamii nchiniTanzania.
Mada ya mjadala huo uliofanyika katika ukumbi wa kimataifa waq mikutano katika jengo la PPF ilikuwa “Mabadiliko ya Katiba ya Nchi Mwaka 2011; Je, mchakato unaopendekezwa utazaa katiba inayotokana na matakwa ya wanachi? Kimsingi jibu kutoka ukumbini lilikuwa hapana!
Mdahalo huo chini ya uenyekiti wa Bi. Rose Mwakitwange uliandaliwa na Tanzania Development Initiative Programme (TADIP), kwa kushirikiana na Konrad Adenaeur Stiftung (KAS), pamoja na kujadili mambo kadhaa muhimu pia ulihudhuriwa na makundi mbali mbali ya wanaharakati na wawakilishi kutoka vyama vya siasa.
Naye meneja wa programu wa TADIP Steven Mmbogo aliwaomba wachangiaji katika mjadala huo wasiwe na woga wowote kwani nchi hii ni mali ya Watanzania wote na hakuna mtu wala kikundi chenye haki miliki ya kuitawala.
“Ninaomba kuwataarifu wanakonagamano kwamba ni lazima tujiridhishea iwapo muswaada huu utakidhi viwango na kama jambo hilo haliwezekani basi tutoe kauli yetu kuashiria jambo hilo .
Miongoni mwa wanakongamano waliokuwapo viongozi wa vyama kama vile Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt Willibrod Slaa, na yule wa chama cha National Convention for Construction and Reforms, Sam Ruhuza.
“Ingawaje Rais Jakaya Kikwete aliahidi kwamba ataanzisha mchakato wa wanachi kujitengenezea katiba mpya lakini uzoefu wa mtindo na lugha iliyotumika unadhihirisha kwamba hapatakuwapo na katiba mpya bali marejeo ya katiba iliyopo, ni juu yenu kumau ni vipi tutasonga mbele katika mchakato huu,” alisema Prof Maina.
Mwanasheria huyo maarufu aliyebobea katiku utaalamu wa katiba alisema wataalamu wa kompyuta wana usemi wa Kiingereza, ‘garbage in garbage out’ ihivyo basi wapo mchakato wenyewe hivi ndivyo ulivyoanza basi unadhihrisha kwamba wananchi hawatapata kile walichokitarajia.
Alisema makelele yaliyojitokeza ukumbini Karimjee na hata Dodoma yanaashiria kwamba wananchi wengi hawajaridhishwa na muswaada ulioletwa na serikali tayari kwa kupokea mawazo ya wadau mbali mbali na wananchi wote kwa ujumla.
Ni baada ya kutoa kauli hiyo ndipo wanakongamano walisikika wakisema “tunapoteza muda, tunataka katiba mpya na wala si kuirejea iliyopo,” ni hapo mwenyekiti alipoomba ushauri wa Prof Maina ambaye alishauri kwamba wananchi wasiache mijadala inayoendelea bali waitumie vizuri zaidi kwa kufikisha ujmbe wao.
Akiirejea historia ya madai ya katiba mpya Prof Maina alisema kilio cha kwanza kikubwa kilianza pale ambapo Tanzania iligeuzwa kuwa nchi ya chama kimoja mwaka 1965, na kuanzia wakati huo kelele hizo zimekuwa zikipotea na kurejea mara kadhaa kulingana na mazingira husika.
Lakini kelele kubwa zilisikika tena mwaka 1984 ambapo vugu vugu hilo lilizimishwa ghafla na kukawa na ukimya kwa mika kadhaa hadi hapo miaka ya mwanzo ya 1990 baada ya kusambaratika dola la iliyokuwa Jamhuri ya Muungano wa Kisovieti, vugu vugu hilo ndilo lililosababisha kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania .
Prof Maina alisema kilio cha sasa cha katiba kimetokana na ukweli kwamba kuanzia mwaka 1992 ni Chama Cha Mapinduzi pekee ambacho kimeendelea kuhodhi madaraka hali ambayo imewanyima Watanzania wengine kushiriki katika mchakato wa kisiasa kwa sababu wagombea binafsi hawaruhusiwe katika nchi hii.
Msomi huyo hakusita kuzirejea tume kadhaa ikiwamo ile ya marehemu Jaji Francis Nyalali, Jaji Robert Kisanga na ambavyo zilishindwa kuleta kile ambacho Watanzania walikitarajia. Alisema moja yapo ya changamoto ya tume hizo ni kule kupangiwa hadidu za rejea na maswali yasiyotoa nafasi kwa wanaojibu kueleza hisia zao.
“Nadhani wanakongamano mnakumbuka jinsi ambavyo Rais Mstaafu Benjamin Mkapa alivyokerwa na kitendo cha Jaji Kisanga kutamka baadhi ya mambo ambayo hayakuwamo katika hadidu za rejea,” alisema Maina.
Mwanazuoni huyo alisema kwamba litakuwa jambo la ajabu iwapo Watanzania hawatadai katiba yao kwa sababu tayari Wazanzibar wamejitengenezea katiba yao ambayo inatambua Serikali ya Umoja Kitaifa ambayo kimsingi imetengua Serikali ya Mapinduzi ambayo katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bado inaitambua.
Naye Bashiru Ally alisema tatizo kubwa hapa Tanzania ni kutaka kutumia sheria ili kuondoa mamlaka ya kisiasa, “sheria na katiba ni lazima vikiji malengo ya kisiasa na wala siyo kugandamiza malengo hayo,” aliseama mhadhiri huyo.
Naye Bw Mmbogo alisema tayari muswaada umeonyesha kupingwa takrin kila mahali pale ulipojadiliwa hali inayoashiria kwamba kuna matatizo au muswada wenyewe haukidhi viwango na kwa maana hiyo hauna tija kwa wanachi.
Naye Dkt Slaa alisema kulingana na unyeti wa mjadala wa katiba ilitakiwa vituo vya mijadala viongezeke ili kuwafikia wananchi wengi zaidi badala ya hali ya sasa ambapo mijadala hiyo ilifanyika Dar es Salaam. Dodoma na Zanzibar . Alisema kwa mtindo mawazo ya wananchi wengi yameachwa nje wakati yangekusanywa yangesaidia katika kupata katiba nzuri zaidi.
Mwisho
No comments:
Post a Comment